LEKIDEA :: TAARIFA YA MAENDELEA TOKA KWA MH. DIWANI, BOQs ZA BARABARA NA MPANGO MKAKATI, KATA KIRUA VUNJO MASHARIKI 2010-2020
Mh.
Diwani Alex J. Umbella (KV.East)
Wapendwa
wana LEKIDEA
Napenda kuvunja ukimya na
kuchukua fursa hii ya pekee kuwashukuru kwa jitihada maalum mlizozitoa kwa
ajili ya maendeleo ya Legho Kirua. Jitihada zilianza na ujenzi wa Kanisa la
Karmel hatimaye zikapata msisimko upya wakati wa ujenzi wa awamu ya kwanza ya
miundombinu ya barabara za Vijiji. Hapana shaka tukio hili la ujenzi wa
barabara lilivuta hisia nyingi toka kwa Jamii na taasisi zinazotuzunguka hasa
ndani ya LEKIDEA, huku baadhi ya watu wakihoji hatma na azma tuliyojiwekea. Kwa
vyovyote vile hatuna budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuvusha na
kutuondolea hofu kwenye changamoto za kisiasa na nyinginezo zilizojitokeza na
hatimaye kutupeleka kwenye Dira ya Maendeleo tuliyojiwekea.
Michango iliyoelekezwa kwenye
ujenzi wa barabara takribani milioni themanini imetujengea heshima kubwa ndani
ya jamii ya wanalegho na Mkoani na hasa ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Moshi
ambako nasimamia na kutetea masilahi ya wananchi wa Kata ya Kirua Vunjo
Mashariki. Ikumbukwe ujenzi wa barabara haukufanywa kwa kificho, nilikaribisha
timu ya Halmashauri ya Wilaya ya Moshi hususan Mkurugenzi Mtendaji, Afisa
Mipango na Mhandisi wa ujenzi kutembelea Kirua Vunjo kuona ni jinsi gani kazi
ilivyokuwa ikifanyika.
Kilichowavutia na kuwashangaza
ni matumizi ya mashine maalum za ujenzi wa barabara ambazo ni nadra sana kuonekana Vijijini
mf. Caterpillar, bulldozer, roller, excarator. Nawashukuru sana kwa uhamasishaji uliofanywa na viongozi
wa LEKIDEA kwani wananchi wenye mashamba yanayopakana na barabara walionyesha
ukomavu wa hali ya juu katika kuyapokea mabadiliko.
Barabara zilizochimbwa,
kuwekwa moram na kushindiliwa kwa roller zimeweza kuhimili vishindo vya mvua za
masika zilizokuwa nyingi na kutikisa sehemu mbalimbali za nchi kwa sababu hiyo,
barabara za Madukani – Kilasanioni, Madukani – Kisanja, Madukani – Kiwelewele
(via kwa W. Matay), na Madukani – Mrumeni (kwa Mkoloni) zimeweza kupitika
kipindi chote cha mvua kwa magari na pikipiki. Kadhalika kiwango cha usafi hasa
wa viatu na mavazi kwa wananchi wetu kimepanda kipindi cha mvua.
Zaidi ya hayo ujenzi wa
barabara uliotekelezwa na LEKIDEA umekuwa wa kiwango kikubwa zaidi kuliko
ujenzi ulifanywa na Serikali. Hii inathibitishwa na ukweli kwamba barabara ya
Uchira – Kisomachi iliyotengenezwa muda mfupi tu kabla ya kuanza kwa ujenzi wa
LEKIDEA iliharibika na kusababisha kukwama kwa magari eneo la Mtemboni na
Msufin. Eneo la Mbuyuni kwa Mtanzania lililorekebishwa na LEKIDEA limebaki kuwa
salama. Hili ni jambo ambalo LEKIDEA inapaswa kujivunia. Mhandisi wa barabara
(W) ameliona hili na wakandarasi wa barabara watatakiwa kuzingatia viwango
pindi wafanyapo kazi katika eneo letu.
Wapendwa
wana LEKIDEA
Serikali nayo haijawa
mbali na juhudi zetu. Mtakumbuka kuwa miaka miwili iliyopita barabara ya Uchira
– Kisomachi ilikuwa mbaya sana,
Serikali ilitoa T.Shs.47,000,000/= kuirejesha mahali pake. Pia zilitolewa
T.Shs.5,500,000/= kutengeneza barabara ya Madukani – Kolaria. Hapo majuzi
Serikali imetoa tena T.Shs.46,550,000/= kwa mkandarasi JABEL INVESTMENT CO. LTD
ya jijini Dar es Salaam. Shughuli hii ya ujenzi ipo katika hatua ya
“mobilization”. Hatuna budi kujenga uhusiano naye atuhakikishie kazi nzuri na ya
viwango! Naambatanisha BOQS kwa kazi hiyo. Wakati huo huo Serikali imetoa
T.Shs.9,300,000/= kwa matengenezo ya barabara ya Nganjoni – Mabungo iliyopo
kwenye Kata yetu. Napenda kuwajulisha kuwa kwa tathmini niliyofanya Kata yetu
inapata fedha nyingi toka kwenye mfuko wa barabara kuliko Kata nyingi za
Halmashauri ya Moshi! Zaidi ya hayo barabara ya Kisomachi – Nganjoni – Masaera
(Kilema) imeingizwa Serikalini. Hii itatuwezesha kupanua uwezo wa soko la
Kileuo badala ya kumtafuta mchawi.
Serikali imetoa
T.Shs.55,000,000/= kwa ajili ya maendeleo ya Shule ya Sekondari Kilimani chini
ya mpango wa TASAF kutokana na fungu hilo
Shule imeweza kununua madawati 100, viti 100, kabati za kuhifadhi vifaa,
kujenga madarasa mawili na vyoo vya wanafunzi. Hata hivyo, madarasa
yamekamilika kwa shida na vyoo kujengwa bila mfumo wa maji kutokana na kamati
ya usimamizi (Mero) kutowajibika ipasavyo. Kwa vyovyote vile udhaifu
uliojitokeza unaanzia kwa wataalamu wachache wasiokuwa waadilifu ndani ya
Halmashauri ya Moshi. Tunafuatilia tatizo hili kwa karibu.
Jengo la Zahanati ya
Kileuo lililokuwa limeanza tangu mwaka 2007 na kuzuiliwa kwa miaka kadhaa
kutokana na usimamizi duni wa Serikali ya Kijiji, mkakati wa ujenzi wa Zahanati
umepata msukumo upya baada ya Serikali kutuma tena T.Shs.20,000,000/= kwa
masharti mapya chini ya uangalizi wa Kata. Tunatarajia kukamilisha ujenzi mwaka
huu na tayari tumeshaingiza Zahanati kwenye mpango wa huduma za Serikali.
Zahanati ya Kileuo imekuwa kikwazo kikubwa kwa ujenzi wa Ofisi ya Kata.
Tumeendelea kuhamasisha
bustani za miche ya kahawa kwa ajili ya wakulima wetu.
Msimu huu chama chetu cha (KNCU)
kimeweza kuzalisha miche 15,000 na kusambaza kwa wakulima wetu. Bei ya mche
mmoja ni shilingi 300. Miche mingi iitolewa kwa mkopo kutokana na hali mbaya
kifedha. Wakulima kadhaa wameanza kunufaika na matunda ya miche bora ya kahawa
ijapokuwa bei ya kahawa imeshuka kwenye soko la dunia.
Tatizo la ukosefu wa ajira
kwa vijana wetu limekuwa kwa kiasi kikubwa na limeanza kutishia maisha ya watu
katika eneo letu. Kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa uongozi wa Kata umewakusanya na
kuwaunganisha vijana katika vikundi vya watu kuanzia 10 hadi 25. Tumewafundisha
namna ya kuandika katiba ya vikundi na kutengeneza andiko la miradi na hivi
karibuni tumetuma maombi ya mikopo Serikalini ili vijana waweze kunufaika na
fungu la Maendeleo ya Vijana. Kutokana na mkakati huu vijana wameweza
kujitambua ndani ya jamii na wengine wameweza kunyoosheana vidole pale
ilipobidi kufanya hivyo. Tunasubiri tuone mwisho wake.
Hapana shaka kuwa mikakati
ya kimaendeleo iliyoanzishwa LEKIDEA imeleta changamoto mbalimbali katika
historia ya maendeleo Kirua Vunjo. Kutokana changamoto hizi, zimejitokeza
harakati mbalimbali ambazo zimeanza kukabili viongozi ambao wameshindwa
kuendana na mahitaji ya sasa ya wanachi. Viongozi / Watumishi walevi, wazembe
wsio waadilifu, wameanza kukumbana na kadhia hii. Tayari Mwenyekiti wa Kijiji
cha Mrumeni amekumbwa na karaha hii. Wimbi linaendelea na hakuna anayejua
mwisho wa siku litakuwaje. Cha msingi ni mabadiliko chanya.
Naomba nisiwachoche sana kwa mawazo yangu
nikaribishe hoja mbalimbali kwa ajili ya kupambana na changamoto zetu za
kimaendeleo katika eneo letu. Mungu aendelee kuwajalia afya na uzima.
Alex J. Umbella
DIWANI
Kata
ya Kirua Vinjo Mashariki.
Aug
2013
No comments:
Post a Comment