LEKIDEA FOCUS OVERVIEW

LEKIDEA
is a registered Non-profit Organization of Kirua Vunjo East Moshi, by Natives from related Villages (Kileuo, Mrumeni, Kotule, Mero, Legho, Lasso, Kwa-Laria(Kanji), dedicated to join together, leverage their Vision, Objectives, Social strengths, ambitions & professionalism and other common resources from members, relatives and families having any origination with K.V East, to come TOGETHER, DEVELOP and CHANGE their Motherland through Projects and involvements in different Social development Initiatives that play roles in alleviating poverty and enhancing opportunities in collaboration with all well wishers, and support from social development entities from the village level, national level, and international level.

Tuesday, November 20, 2012

LEKIDEA: KIKAO CHA HIVI KARIBUNI NA KAZI INAYOENDELEA KV




 LEGHO-KIRUA DEVELOPMENT ASSOCIATION

KIKAO CHA DHARURA CHA SEKRETARIAT NA UONGOZI WA LEKIDEA -26/10/2012

Double Views Hotel – Sinza DSM

KUTATHMINI HALI YA MAENDELEO YA BARABARA
 ------------------------------------------------------
Agenda
1.       Kufungua Kikao
2.       Hali ya Sasa – Current situation
3.       Hatua zinzofuata - Way Forward
4.       Barabara ndogo za Vitongoji - Periphery Roads
5.       Uzinduzi  Rasmi wa Mradi
6.       Michango
7.       Mengineyo
 ------------------------------------------------------
1.       Kufungua kikao
-Kikao kilifunguliwa saa 1:30 jioni kwa sala na Ndg.Joseph Shewiyo – Katibu wa LEKIDEA.
2.       Taarifa ya Hali ya Sasa toka KV.
Utangulizi:
-Mwenyekiti  alianza kwa kuwashukuru wajumbe wote ambao tangu kuanzishwa kwa LEKIDEA hadi sasa wamekua wanajitoa kwa kila hali bila kuchoka na kuhakikisha miradi ya LEKIDEA inasonga mbele bila kukwama hasa katika ujenzi wa barabara, ugumu wowote unaotokea wanabuni mbinu mpya katika kukwamua. Aliwashukuru hususan Martin, Saluo, Shewiyo, Paul, na pia ma-engineer Benin na Njau. Alimalizia kuwa Mungu awabariki sana kwa uvumilivu na kujituma kwao kwa faida ya LEKIDEA na jamii nzima ya KV Mash.

3.  Taarifa Fupi toka KV:
Ø  Martin Kessy alitoa taarifa fupi ya hali ya uwekaji wa Moram iliyoanzia maeneo kadhaa ya Mradi wetu kama ituatavyo:
·         Kiwelewele hadi kwa Matay.
·         Kisanja hadi Kisomachi
·         Kilasanioni hadi kwa Kikuyu-Kitaarinyi
·         Mrumeni hadi Kisomachi.
·         Pendekezo lilitolewa kujumuisha ya njia ya kuanzia Kitaarinyi hadi Kisomachi

Ø  Jumla hadi siku ya kikao, idadi ya malori 200 yalikwishawekwa kwa gharama ya kiasi cha sh.24,000,000  ila zimelipwa trip 100 tu imebaki deni trip 100 ambayo katika Mil 24 zilizopo sasa kiasi cha Mil 12 kitatumika kulipia hayo malori 100. Tutabakiwa na  mil.12 ambazo zinatakiwa kufanya kazi ya kusambaza, kumwagia maji na kushindilia. Aidha zinatakiwa pia kumalizia maeneo matano muhimu ambayo ni barabara ya kutoka Uchira, Kitaarinyi hadi Kisomachi, Kiwelewele hadi Mkombenyi, Kitaarinyi hadi kwa Erene na KNCU Usangi hadi Kilasanioni  

4.       Hatua Inayofuata:
Ø  Kutokana na hali halisi, kiasi kilichosalia ni  12 mil. Michango zaidi inahitajika haraka ili kazi iendelee kwa kasi bila kusimama.
Ø  Zipo trip kama 24 katika hizo mia mbili ambazo bado hazijawekwa. Imeshauriwa kuwa tumkope mwenye Malori trip nyingine 50 ili zitoshe kuweka moram katika barabara zifuatazo ambazo bado:
·         Kitaarinyi kupitia Usangi  hadi Kilasanioni.
·         KNCU hadi kwa-Rene
·         Kwelewele hadi Lasso - Juu (Mkombenyi)
·         Kitaarinyi hadi Kisomachi
·         Kisomachi hadi Uchira (pale Juu ya Maweni na Kiorotsuni)

Ø  Pia imependekezwa  kuwa Doza  litengenezwe haraka ili kumalizia barabara za KNCU hadi Kwa-Rene na KNCU hadi Usangi -Kilasanioni

Boza, Greda na Compactor: 
Ø  Imependekezwa ipatikane haraka Boza, Greda na Compactor  kushindilia njia zote  zilizokwisha fanyika usambazaji wa Moram.
Ø  Secretariet itawasiliana na  Wahandisi Ben na Njau walioko KV ili kutathmin hali ya njia na maeneo  ya ndani watakayohitaji Culverts  na ushauri mwingine wowote ili kuimarisha kazi iliyokwishafanyika.
.
5.       Barabara za Vitongoji – Periphery Roads
Ø  Ufafanuzi ulitolewa kuwa barabara zinazojengwa na Lekidea ni zile zilizoainishwa katika mradi mkuu ambazo zinaunganisha vijiji vyote vya eneo hilo. Pia zile zinazokwenda kwenye vyama vya ushirika vya msingi na mashule.
Ø  Barabara ndogo ziingiazo ndani ya vitongoji, zimewekwa kama ‘Peripheral  roads’ za Lekidea ambazo LEKIDEA haitaweza kufanyia kazi katika mradi huu mkuu bali familia zinazotumia barabara hizo ndogo zikipenda  watachanga kwa ajili ya ukarabati wa njia hizo specific na LEKIDEA inaweza kusaidia usimamizi zikatengenezwa ipasavyo. Hivyo ieleweke kuwa  barabara  ndogo ndani ya vijiji au vitongoji, watachangia  wahusika watumiaji wa njia hizo na LEKIDEA inaweza kusimamia kazi husika.

6.       Uzinduzi Rasmi
Ø  Lilitolewa pendekezo kuwa aombwe Kiongozi fulani afungue barabara zetu. Wazo hili lilikubalika kwa kiasi ila litahitaji kupata maoni ya wajumbe wengine.
Ø  Kutokana na shughuli hii ya Uzinduzi kuwa muhimu sana, ilipendekezwa Ndg Venance Msaki pamoja na Savinus Kessy watasaidia kuonana na Ndg Dennis Msacky (wa Mwananchi) ili awezeshe kumwona Mgeni aliyependekezwa pindi tutakapo kubaliana katika hatua hii. Mgeni rasmi huyo wa ufunguzi atakuwa muhimu kwetu katika suala zima la Fund-Raising kwa ajili ya miradi inayoendelea ambayo ni ya kufufua zao la Kahawa na kupanda miti na Mazingira.
Ø  Pia pendekezo la kumtumia Ndg Dennis Msacky kuweka Makala ya Miradi na majukumu ya LEKIDEA katika gazeti la Mwananchi aliachiwa V. Msaki alifuatilie.
  
7.       Michango.

Ø  Martin alitoa taarifa fupi  ya michango ambayo  imeshaelezwa juu  ni mil.24. Ukipunguza deni la trip 100 ambazo ni sh.12,000,000, baki ni 12,000,000. Michango zaidi inatakiwa kuwezesha Moram kuendelea.

Ø  Taarifa ya Makusanyo na Matumizi hadi siku ya Kikao
Taarifa kama ilivyowasilishwa na Ndg Emilian Saluo ilikuwa kama ifuatavyo:
·         Makusanyo Jumla ni Sh 65,866,626/-
·         Kiasi cha hela haijaja  ni 26,746,000.
·         Jumla ya matumizi ni 42,860,410
·         Balance kufikia leo  24,100,000

Kiasi kinachokuwa bado kinadaiwa toka kwa wachangiaji  ni 26,746,000 ambayo inatoka  kwa waliokwisha ahidi, fedha ambayo inahitajika kukusanywa mapema sana ili kumaliza kazi iliyosalia. Ilionekana kuwa hawa walioahidi na bado kutoa fedha wanakwamisha malengo yetu. Imekubalika kwa majina yote yachujwe  yatangazwe kwa jamii yetu. Iliafikiwa kuwa majina  hayo yawasilishwe kwa Bw  Njau ili awasilishe  kwa Paroko ayatangaze kanisani  ili jamii iwatambue wagumu hao.
 
8.        Mengineyo.

Ø  Michango iendelee kuhamasishwa kwa SMS , hii iliafikiwa kuwa iwepo  njia ya kutuma SMS  kwa kila mdau. Uwepo muda fulan ambapo kikao kikiafiki fedha kiasi  zitatoka kulipia central-SMS ambayo atatumia Paul Msaki  kusambaza SMS kwa mtandao, Secretariet  itajadili.
Ø  Pia ilipendekezwa kuwa sms fupi  na nzuri iandaliwe  itumwe kwa wote hasa wale ambao  wanagoma, ili angalau watoe kiasi chochote na kila apataye SMS hiyo aisambaze pia kwa wengine .

Kikao kilifungwa saa 3:15 usiku kwa sala

Waliohudhuria-
1.       Edward Msaky – M/Kiti - LEKIDEA
2.       Joseph Shewiyo – Katibu -
3.       Martin M Kessy
4.       Paul Msaki
5.       Thomas Msaki
6.       Savinus Kessy
7.       Venance V Msaki



--------------------------------------            --------------------------------------
Katibu                                                    M/Kiti
LEKIDEA


---------------------------------------------------------------------

 ZIFUATAZO NI  BAADHI TU YA PICHA ZA MATUKIO YA UJENZI KATIKA MAENEO MBALIMBALI YA BARABARA ZETU ZA LEGHO-KIRUA VUNJO MASHARIKI, MRADI UNAOSIMAMIWA NA TAASISI YETU YA LEKIDEA.

---------------------------------------------------------------------

Kwa dhamira moja, kazi ya kuchonga Barabara zote muhimu kama zilivyoainishwa katika 'Mradi Mama' wa LEKIDEA zilianza kwa kasi kubwa pasipo kizuizi chochote kikubwa, na kulingana na malengo na matarajia, kazi ya uchongaji ilikamika vyema kama inavyoonekana pichani juu, hii ikiwa ni sehemu ya barabara ielekeayo Kisanja-Legho KV.
Hii ni sehemu muhimu ya Makutano ya 'Kitaarinyi' katika Barabara ya kutoka Kisomachi hadi KNCU au Mero Kati. Barabara imefanyiwa kazi bora, na hapa inaonekana Greda lilisambaza Moram na kusawazisha vyema.
Baada ya Kazi kubwa ya Greda kuchimba, kusawazisha na kusambaza Moram uliomwangwa katika barabara zetu, kazi muhimu ni ya kushindili. Hapa linaonekana 'Shindilia' likifanya kazi yake na kuimarisha zaidi dhidi ya mmomonyoko.


Maeneo mengine mengi kazi zimefanyika kwa kujitolea na kwa kiwango bora sana. Hapa inaonekana Greda likisambaza Moram na kuweka mikondo ya kuelekeza maji ya mvua pembeni ili yasiharibu barabara. Vijana wetu wanaonekana wakipita kwa hamasa wakishuhudia kazi iliyokuwa inaendelea
Kazi ya nguvu inaendelea, kusambaza na kusawazisha Moram. Pamoja na kazi ikiendelea, wananchi walikuwa wakiendelea kufaidika na huduma hii muhimu ya barabara kwa walio na usafiri binafsi na pia mama zetu waendao mashambani, sokoni na maeneo mengine ya huduma za jamii. Hakika maendelea yanakuja vyema.


KAZI ZAIDI ZINAENDELEA,  UWEKAJI NA USAMBAZAJI WA MORAM KATIKA NJIA ZOTE MUHIMU, IKIWA NI PAMOJA NA KUKARABATI MAENEO KOROFI ENDAPO MVUA ZITALETA HITILAFU YOYOTE, HAYA YOTE TATAFANYIKA VYEMA.

KADHALIKA, NJIA ZA VITONGOJI PIA ZIMEPEWA KIPAUMBELE HASA KWA MICHANGO YA WAZALIWA WA MAENEO HUSIKA (AU FAMILIA) AMBAPO NJIA HIZO ZINAPITA. WANAWEZA KUJIUNGA NA KUCHANGIA KWA PAMOJA KUIMARISHA MAENEO YAO. WACHANGIAJI WANAWEZA KUCHANGA NA KUELEKEZA KUWA 'MCHANGO WANGU/WETU WA GREDA/MORAM AWAMU HII UKAFANYIE KAZI KATIKA NJIA AU MTAA/KITONGOJINI KWETU'...LEKIDEA IPO TAYARI NA ITAJITAHIDI KUTIMIZA HILO KULINGANA NA UMOJA WA WAHUSIKA NA HALI HALISI NA KIWANGO CHA WACHANGIAJI HAO ILI KUTOKUSABABISHA TATIZO.
TUCHANGAMKE, MUDA NDIO SASA, KUJENGA ASILI YETU.

PAMOJA TUTAFIKA NA KUFANIKIWA. TUUNGANISHE NGUVU!
TUCHANGIE BILA KUKATA TAMAA, NI MAENDELEO YETU WENYEWE.

---------------------
Michango ya LEKIDEA inaweza kuwasilishwa kwa CASH au kwa njia zifuatazo.
CRDB A/C: 0152095786500; 
LEGHO KIRUA DEVELOPMENT ASSOCIATION
Kwa Simu: Vodacom MPESA– 0755 799 133; TigoPESA- 0653 799 133

Muda ndio sasa, TUCHANGIE, TUENDELEE MBELE!!.

TYK...
Secretariat - LEKIDEA
 








Sunday, August 5, 2012

KIKAO CHA LEKIDEA 22-07-2012 NA TAARIFA RASMI

Wapendwa Wana-LEKIDEA, na Wapenda Maendeleo wote wazaliwa wa Ukanda wa Legho-Kirua Vunjo Mashariki, na Wapenda maendeleo wote popote walipo Tanzania na Dunia Nzima. Salaam ziwafikie!

Uongozi wa Taasisi yetu muhimu ya Legho-Kirua Develeopment Association (LEKIDEA), hivi karibuni (22/07/2012) ulifanya Kikao Muhimu cha kufuatilia mambo muhimu na Utekelezaji wa Miradi iliyo katika Mikakati na Malengo ya Taasisi hii muhimu inayolenga kunyanyua maisha ya Eneo walilozaliwa la Legho-Kirua Vunjo Mashariki. Kikao kilikuwa cha manufaa sana.

Pamoja na Mambo mengine muhimu, Kikao hiki kilichoongozwa na M/Kiti wa Taasisi Ndg Edward F. Msaky, kilikuwa cha mafanikio makubwa, na kiliweza kujenga midani na mikakati bora kabisa katika kuifanya Taasisi kutimiza malengo yake na majukumu muhimu iliyojiwekea katika kuukomboa ukanda wetu katika hali ya 'kusahaulika' kimaendeleo na kiuchumi. Baadhai ya masuala muhimu yaliyofanyiwa kazi ni pamoja na Kufuatilia kwa umakini Mradi wa Ukarabati wa Barabara za Vijiji vyote vya Legho-Kirua Vunjo, (kama ilivyoainishwa katika Taarifa Rasmi kwa Vyombo vya Habari 'Press Release' chini) ambapo Mradi wenyewe ulishaanza. 

Pia mikakati mingine katika Kikao ilihusu uhamasishaji zaidi wa wazaliwa wote wa maeneo ya Legho-Kirua Vunjo Mashariki popote walipo ili waweze kuungana zaidi na kuchangia kwa hali na mali katika kuhakikisha maendeleo yaliyokusudiwa kwa kupitia taasisi hii ya LEKIDEA inafanikiwa kwa kiwango kikubwa ili kufaidisha wananchi wote wa sasa na vizazi vijavyo. 

Kadhalika, suala muhimu la kuwafahamisha wanachama wote wa Legho-Kirua, Tanzania nzima na wapenda maendeleo wote, hali halisi na maendeleo ya Michango ya wanachama, Miradi na malengo ambayo yalikwishafikiwa hadi sasa, ili kwa njia moja au nyingine waendelee kuhamasishana kila mwanachama na kuutambua umuhimu wa kuunga mkono juhudi hizi za LEKIDEA, kadhalika na taasisi za ndani na nje ya nchi ambazo zinathamini hatua na juhudi hizi za maendeleo kwa ngazi ya chini (vijijini) zinazofanywa na LEKIDEA, na juhudi zilizokwishafanyika hadi sasa, wapate kutuunga mkono na kuchangia maendeleo yetu kwa hali na mali kwa kupitia Taasisi yetu hii Rasmi iliyosajiliwa kwa malengo na dhamira ya kuukomboa ukanda wetu kiuchumi, kijamii na yote yanayohusika nayo. Dalili ni njema sana na yafaa kutuunga mkono, na haraka tutasonga mbele zaidi.

Chini hapa ni baadhi ya Picha za matukio kadhaa muhimu zitokanazo na Kikao hicho:

Kutoka kushoto: Mwenyekiti wa LEKIDEA, Ndg Edward Msaky, akipitia kwa umakini taarifa na oradha ya mambo muhimu yaliyokuwa yakijadiliwa katika kikao. Katikati ni Katibu wa LEKIDEA Ndg Joseph Shewiyo akifafanua agenda kwa Wajumbe, na kulia kwake ni Makamu M/Kiti Eng. Simon Njau, akipitia baadhi ya majina ya Wanachama katika Simu yake katika kuwasiliana nao yale yanayoendelea katika kikao.

Kutoka kushoto: Mjumbe wa Kikao Mh. Adocate Minja, na katikati ni Eng. Bernard Ndepachio Msacky, na kulia kwake ni Mwanasheria wa Taasisi, Wakili Tonny Teye, wakisikiliza kwa makini maendeleo ya agenda katika kikao.
Wajumbe wa Kikao cha LEKIDEA, kutoka kushoto; Ndg Emilian Saluo Assey, akifuatiwa na Ndg Venance V. Msacky, akifuatiwa na Ndg Amani-Ereney Beda Kyara na wa mwisho kulia ni Ndg Gabriel Kessy, wote wanaonekana wakifuatilia kwa makini agenda za kikao zilivyokuwa zikifafanulia.
Wajumbe wa Kikao cha LEKIDEA, kutoka kushoto; Ndg Paul Sanene Z Msaki, akifuatiwa na Ndg Martin Mathias Kessy, ambaye pia ni Makamu-Katibu wa LEKIDEA, na mwicho kulia ni Ndg Emilian Saluo Assey wakisikiliza kwa utulivu masuala muhimu ya utekelezaji kama yaliyokuwa yakielezwa toka meza kuu.
Katika picha juu, anaonekana Katibu Mkuu wa LEKIDEA Ndg Joseph Ignas Shewiyo anachambua vipengele muhimu kutoka katika agenda zinazojadiliwa na kulia kwake M/Kiti, Ngd Edward Msaky akifuatilia sambamba na Makamu-M/Kiti Eng. Simon Njau akiendelea kuwasiliana na baadhi ya wajumbe katika kufanikisha uchangiaji.
Pichani: Toka kushoto, Makamu Katibu wa LEKIDEA Ndg Martin Kessy akifuatiwa na Ndg Emilian Saluo Assey na kulia kwake ni Ndg Amani-Ereney Kyara, wote wakisikiza na kufuatilia maendeleo ya kikao.
Hiki ndicho kikosi kamili kilichoketi katika kikao hicho muhimu kwa masaa karibia manne bila kuchoka, na kufanuikisha majukumu na masuala muhimu sana ya kiutekelezaji ambayo ndiyo msingi wa LEKIDEA na jamii nzima kuendelea kusonga mbele. Ari, moyo wa kujitolea na umahiri wao katika kufuatilia utendaji ndio dira na nguvu ya LEKIDEA ambayo kila mmoja wetu na yeyote mpenda maendeleo yafaa kuunga mkono. Kuoka kushoto waliosimama: Ndg Venance V Msacky, Ndg Gabriel Kessy, Mh Advocate Minja, Ndg Paul Sanene Z. Msaki, Ndg Emilian Saluo Assey, Ndg Amani-Ereney Beda Kyara, Eng Bernard D. Ndepachio Msacky, na Ndg Tonny Teye. Waliokaa, kuanzia kushoto:  Ndg Martin Mathias Kessy, Ndg Edward F. Msaky, Ndg Joseph Ignas Shewiyo na Eng Simon T Njau. Mjumbe mmoja Ndg Sylvester A. Matemu (hayupo pichani) aliwahi kuondoka kutokana na majukumu ya dharuara yaliyomlazimu kuwahi kuondoka.
 -------------------&&&----------------------

WAPENDWA WANA-LEKIDEA, NA WANANCHI WOTE WENYE MAPENZI MEMA YA KIMAENDELEO, HII HAPA NDIYO TAARIFA RASMI YA LEKIDEA KAMA ILIVYOTOLEWA KATIKA GAZETI THE GUARDIAN LA TAREHE 03/08/2012.


MWANA-LEKIDEA, TUENDELEE KUCHANGIA MAENDELEO YETU PASIPO KIKWAZO, AU KUKATISHWA TAMAA NA MTU AU KIKUNDI CHOCHOTE, MAANA KUDHOOFU KWETU NDIO MTAJI KWA WENGINE, NA TUJITAMBUE DAIMA KUWA MAENDELEO YETU YATALETWA NA SISI WENYEWE, ....NA WAKATI NDIO SASA!! TUUNGANISHE NGUVU!

Friday, March 23, 2012

LEKIDEA: MRADI WA BARABARA ZA VIJIJI - AWAMU YA 1:

Ndugu wana-LEKIDEA

Tunawasalimu wote tena kwa Jina la Mwenyezi na tunawapa pole kwa majukumu mengi ya mwaka mpya.
Kama mjiavyo, Sekretariet imekuwa inafanya kazi juu chini kuhakikisha kuwa jambo muhimu tulilolianza linatekelezwa kama inavyotakiwa.
Awali tulitegemea hatua za Halmashuri yetu lakini baada ya kuona kuwa zinachelewa Sekretariat imeandaa 'mpango-kazi' wa utekelezaji kwa barabara zetu za, kule juu kuanzia Kisomachi kwenda Vijijini. Wote tuelewe kuwa kwa kuwa hatuna mamlaka ya kutengeneza barabara ya Uchira-Kisomachi bila kupitia Halmashauri, ndiyo maana hatujaiweka katika mpango huu wa awamu hii ya sasa.
Halmashuri itakapoanza ujenzi sisi bado tutaingia humo kama tulivyoahidi na kufafanua katika mpango wa kwanza. Kwa sasa tunapendekeza utekelezaji uwe kwa LEKIDEA kukubaliana na Mkandarasi wetu kuanza ujenzi wa barabara za vijiji zifuatazo zenye jumla ya kilomita 12 (tazama barabara nyekundu kwenye ramani iliyoambatanishwa chini).

BARABARA HUSIKA - AWAMU YA 1:
- Kisomachi hadi Kwa-Laria kupitia Mero Kati
- Kwa-Matay hadi Laso juu (Mkombenyi) kupitia Manzaoni-CCM na Kiwelewele
- Kisomachi hadi Kapero Center
- Kisomachi hadi Shule ya Kilimani kupitia Mrumeni
- Kitaarini hadi KNCU


Ndugu wana LEKIDEA wote, kama mnavyoona kwenye jedwali la gharama tunaweza kuanza ujenzi kwa hatua (1) (ktk Jedwali), ambayo ni kujenga mitaro ya maji na culverts, Ili tuweze kuendelea na kuchonga barabara hizo (grading) namba (2), kwa kiwango stahiki tutahitaji kubanana sana walikwishatoa pledge tunawaomba wakamilishe na ambao bado wote tuungane watoe michango yao, na wote tuhimizane kwa nguzu zote. 
Nia yetu ni kukamilisha hadi namba (3) ksms inavyoonyeshwa katika Jedwali, ambayo ni Moram na compaction ni gharama kubwa lakini tunataka kila mtu ajitoe hasa wale wengi ambao bado. Kadahalika tumewaomba wazazi waliopo katika Vijiji vyote, wahimize watoto wao na wao wenyewe washiriki.
Tunatafuta ushauri wa wataalamu kuhusu mvua za masika kama ni busara kuanza kabla au baada ya mvua. Hata hivyo utekelezaji ni lazima, tumeanza lazima tufike. Sasa tunaomba maoni yenu katika vipengele vyote ikiwa ni pamoja na namna ya kupata fedha ya kutosha kukamilisha kazi hiyo muhimu katika hatua hii tunayotaka kuchukua sasa.
Tunawategemea sana Ngd Wafuatao katika kufuatilia na kutoa Mwongozo na Uangalizi katika mradi huu muhimu: Eng Bernard D. Msacky, Eng. Simon Njau, Eng.Bona na tunatangulia kuwashukuru WOTE kwa kufanya kazi hii endelevu na iweze kufanikiwa vyema. 
Tunawaomba wote kutoa maoni na mawazo endelevu mapema NDANI YA WIKI MOJA, ili kufikia muafaka ma kuwezesha mradi huu kuanza.
PAMOJA DAIMA, TUTAFANIKIWA HARAKA.

TYK......,
SEKRETARIAT - LEKIDEA,
 ------------------------------------------------------------------------------------------

RAMANI YA BARABARA HUSIKA KATIKA AWAMU HII:

MAKISIO YA GHARAMA KWA AWAMU HII YA 1